Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bayt AS amesema kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu kupitia vitendo kama vile kuchoma moto Qur'ani ni katika njama za maadui za kukabiliana na Qur'ani Tukufu na Uislamu. Ayatullah Abbas-Ali Akhtari ameongeza kuwa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Uingereza zinatekeleza njama za kuzuia kuenea Uislamu duniani.
Ayatullah Akhtari ameyasema hayo siku ya Jumatano mjini Tehran katika khitma iliyoandaliwa kwa ajili ya watu wa Afghanistan waliouawa shahidi katika maandamano ya kulaani kitendo cha Wamarekani kuchoma moto nakala kadhaa za Qur'ani Tukufu nchini humo hivi karibuni.
Ayatullah Akhtari ameelezea masikitiko yake kuwa wahubiri katika kasri ya mfalme anayejiita kuwa ni Khadimul Haramein wanalinda maslahi ya Marekani na kuunga mkono jinai za dola hilo la kiistikbari.
Amesema ni jambo la kusikitisha kuona wahubiri hao wakipuuza kitendo cha Wamarekani kuchoma moto Qur'ani na hata hawako tayari kutoa fatwa kuhusu suala hilo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bayt AS ameongeza kuwa ni jukumu la kila Muislamu kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu. Ayatullah Akhtari amesema, 'Maadui wafahamu kuwa Waislamu hawatastahamili jinai dhidi ya matukufu ya Kiislamu na kwamba watakabiliana vikali na suala hilo.
No comments:
Post a Comment