Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jeshi la Kiislamu linalochunga mafundisho ya Mwenyezi Mungu na lipo kwa ajili ya kulinda manufaa ya taifa.
Ayatullahil Udhma Khamenei ambaye ndiye Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran amesema leo hayo mbele ya makamanda wa kikosi cha nchi kavu cha jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuhoji akisema, jeshi la Marekani ambalo linaua raia huko Iraq na Afghanistan na kufanya jinai nyinginezo katika nchi hizo, vipi litadai kuwa linatumikia manufaa ya wananchi wa Marekani?
Amesisitiza kuwa, jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndilo jeshi pekee linalotumikia manufaa ya taifa lake na kwamba imani, itikadi na hisia za maafisa na makamanda wa jeshi hilo ndizo zile zile za wananchi wa Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ni jambo la dharura kuendelea kuwepo moyo wa muqawama ndani ya vikosi vyote vya ulinzi vya Iran na kuongeza kama ninavyomnukuu: Tab'an makamanda wa jeshi nao sambamba na kujipamba kielimu na maarifa na kutia nguvu imani zao, wanapaswa pia kuwa na moyo wa ikhlasi na kujiweka mbali na mambo ya kidunia.
Aidha ameashiria madai ya madola ya kibeberu yanayojigamba kuwa majeshi yao yameundwa kwa ajili ya kulinda manufaa ya mataifa yao na kuongeza kuwa, tofauti na madai ya madola hayo ya kibeberu, majeshi hayo hayajali hata kidogo mataifa yao ghairi ya kutafuta jaha na uluwa wa kisiasa pamoja na kuzilinda tawala za kitaghuti.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema, sababu inayoyafanya madola ya kibeberu kutoa vitisho na kuiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kutokana na Iran kuwa kigezo kikuu cha harakati ya kupinga ubeberu na mgawanyo wa kidhulma wa nchi za dunia yaani kugawanywa mataifa ya dunia kati ya yale ya kibeberu na yale yanayopaswa kufanyiwa ubeberu.
Amesema madola ya kikoloni na kibeberu yanaiogopa sana harakati hiyo inayozidi kuenea ulimwenguni na kuongeza kuwa, moja ya sababu zinazoongeza hofu ya maadui ni kufanikiwa vijana wa Iran kuwa kigezo cha mataifa mengine kutokana na kujipamba kwao kiimani, muono wa mbali, maarifa na kuipenda dini na taifa lao.
No comments:
Post a Comment